Isaiah 47

Anguko La Babeli


1 a“Shuka uketi mavumbini,
ee Bikira Binti Babeli;
keti chini pasipo na kiti cha enzi,
ee binti wa Wakaldayo.
Hutaitwa tena mwororo wala wa kupendeza.

2 bChukua mawe ya kusagia, usage unga,
vua shela yako.
Pandisha mavazi yako, ondoa viatu vyako,
vuka vijito kwa shida.

3 cUchi wako utafunuliwa
na aibu yako itaonekana.
Nitalipa kisasi;
sitamhurumia hata mmoja.”


4 dMkombozi wetu: Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake;
ndiye yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.


5 e“Keti kimya, ingia gizani,
Binti wa Wakaldayo,
hutaitwa tena malkia wa falme.

6 fNiliwakasirikia watu wangu
na kuaibisha urithi wangu;
niliwatia mikononi mwako,
nawe hukuwaonea huruma.
Hata juu ya wazee
uliweka nira nzito sana.

7 gUkasema, ‘Nitaendelea
kuwa malkia milele!’
Lakini hukutafakari mambo haya
wala hukuwaza juu ya kile kingeweza kutokea.


8 h“Sasa basi, sikiliza, ewe kiumbe mpenda anasa,
ukaaye mahali pako pa salama,
na kujiambia mwenyewe,
‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.
Kamwe sitakuwa mjane,
wala sitafiwa na watoto.’

9 iHaya mawili yatakupata, kufumba na kufumbua,
katika siku moja:
kufiwa na watoto, na ujane.
Yote yatakupata kwa kipimo kikamilifu,
ijapokuwa uchawi wako ni mwingi,
na uaguzi wako ni mwingi.

10 jUmeutegemea uovu wako,
nawe umesema, ‘Hakuna yeyote anionaye.’
Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza
unapojiambia mwenyewe,
‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’

11 kMaafa yatakujia,
nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi.
Janga litakuangukia,
wala hutaweza kulikinga kwa fidia;
msiba mkuu usioweza kuutabiri
utakujia ghafula.


12 l“Endelea basi na uaguzi wako,
na wingi wa uchawi wako,
ambao umeutumikia tangu utoto wako.
Labda utafanikiwa,
labda unaweza ukasababisha hofu kuu.

13 mUshauri wote uliopokea umekuchosha bure!
Wanajimu wako na waje mbele,
wale watazama nyota watabiriao mwezi baada ya mwezi,
wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu.

14 nHakika wako kama mabua makavu;
moto utawateketeza.
Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe
kutokana na nguvu za mwali wa moto.
Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu yeyote joto;
hapa hakuna moto wa kuota.

15 oHayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi,
hawa ambao umetaabika nao
na kufanya nao biashara tangu utoto.
Kila mmoja atatoroka;
hakuna yeyote awezaye kukuokoa.
Copyright information for SwhKC